IQNA

Mgogoro wa Sudan

OIC yajadili mgogoro wa Sudan katika kikao cha dharura Jeddah

16:33 - May 04, 2023
Habari ID: 3476957
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imeitisha kikao cha dharura nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kuzungumzia mgogoro wa Sudan.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu yenye makao yake makuu mjini Jeddah Saudia Arabia iliitisha kikao hicho dha dharura jana (Jumatano) kujadili hali ya Sudan.

Hissein Brahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC amesema kuwa, kikao hicho cha Kamati Kuu ya OIC kimejadilia upya matukio ya Sudan na kuendelea migogoro ya umwagaji damu kwa zaidi ya wiki mbili kati ya Jeshi na Kikosi cha Radiamali ya Haraka.

Amesema: Mkutano huo umeonesha umakini wa nchi wanachama na ufuatiliaji wao wa matukio ya hivi sasa ya Sudan na nia yao ya kurejesha usalama na utulivu wa nchi hiyo ya Kiarabu ambayo ni mwanachama wa OIC.

Kwa mara nyingine ametilia mkazo ombi lake la usitishaji vita wa kudumu nchini Sudan na kuyapa nafasi mazungumzo na njia sahihi za kudumisha usalama na amani ya watu wa Sudan. Amehimiza pia kuundwa serikali yenye nguvu na yenye uwezo wa kuanzisha tena michakato ya kisiasa nchini na kuelekea kwenye serikali ya kiraia nchini humo.

Leo Alhamisi mapigano makali yameripotiwa kuendelea huko Khartoum, Sudan, huku jeshi likijaribu kurudisha nyuma Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kutoka karibu na ikulu ya rais na makao makuu ya jeshi, licha ya  pande mbili hasimu kudaiwa kusitisha mapigano kwa siku saba katika mzozo huo uliozuka Aprili 15.

Mashambulizi makubwa ya mabomu pia yaliripotiwa siku ya Alhamisi katika miji dada ya Khartoum ya Omdurman na Khartoum.
Ripoti za Sudan Jumanne zilisema watu 550 wamekufa na watu 4,926 wamejeruhiwa hadi sasa katika mzozo huo.

Pande hizo zinaonekana kupigania udhibiti wa maeneo katika mji mkuu kabla ya mazungumzo yoyote yanayowezekana, ingawa mahasimu hao wawili - mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye pia ni mtawala wa Sudan  na kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan "Hemedti" Dagalo - wameonyesha nia ndogo ya kufanya mazungumzo.

Umoja wa Mataifa, wakati huohuo, ulishinikiza pande zinazopigana za Sudan siku ya Jumatano kuhakikisha upitishaji salama wa misaada ya kibinadamu baada ya lori sita kuporwa.

Mkuu wa misaada ya Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alisema anatumai kuwa na mikutano ya ana kwa ana na pande zinazozozana nchini Sudan ndani ya siku mbili hadi tatu ili kupata dhamana kutoka kwao kwa misafara ya misaada.

4137402

Kishikizo: sudan oic burhan dagalo
captcha