IQNA

Taharuki Sudan baada ya mapigano kuzuka Khartoum kati ya jeshi la nchi na kikosi cha radiamali ya haraka

22:59 - April 15, 2023
Habari ID: 3476873
TEHRAN (IQNA)- Milio ya risasi na milipuko imesikika katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, baada ya siku kadhaa za mvutano kati ya kikosi cha radiamali ya haraka na jeshi la nchi hiyo.

Taharuki imetanda baada ya mapigano karibu na makao makuu ya jeshi katikati mwa jiji. Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kinasema kimechukua udhibiti wa uwanja wa ndege na ikulu ya rais. Hata hivyo madai haya yamekanushwa na jeshi.

Awali, kikosi cha RSF kilisema kwamba moja ya kambi zake kusini mwa Khartoum imeshambuliwa.

Kwa upande wake jeshi limesema kuwa wapiganaji wa RSF wamekuwa wakijaribu kuyateka makao makuu ya jeshi.

"Wapiganaji wa kikosi cha (Rapid Support Forces) walishambulia kambi kadhaa za jeshi huko Khartoum na mahali pengine karibu na Sudan," shirika la habari la AFP linamnukuu msemaji wa jeshi Brig Jenerali Nabil Abdallah akisema.

"Mapigano yanaendelea na jeshi linatekeleza wajibu wake wa kulinda nchi."

Duru za habari pia zinawanukuu mashuhuda wakisema kuwa kulikuwa na milio ya risasi katika mji wa kaskazini wa Merowe.

Televisheni ya Alarabia inaonyesha picha za moshi unaotoka katika kambi ya kijeshi huko, shirika la habari la Reuters limesema. Majenerali wamekuwa wakiendesha nchi, kupitia kile kinachoitwa Baraza Kuu, tangu mapinduzi ya Oktoba 2021.

Kikosi cha RSF iko chini ya amri ya makamu wa rais wa baraza hilo Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo. Jeshi, wakati huo huo, linaongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa Baraza Kuu. Hatua iliyopendekezwa ya kufikia serikali ya kiraia iliyopo kwenye ratiba ni kuunganisha kikosi cha RSF katika jeshi la kitaifa. 

3483211

Kishikizo: sudan jeshi
captcha