IQNA

Tahariri

Sababu za malumbano ya sasa ya kijeshi nchini Sudan

21:18 - April 16, 2023
Habari ID: 3476879
TEHRAN (IQNA)- Nchini Sudan hali si shwari ambapo habari kutoka nchini humo zinaonyesha kuendelea mapigano kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya radiamali ya haraka na kuzusha wasiwasi wa kutokea mapinduzi katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Mapigano hayo yaliyoanza jana yameingia siku yake ya pili leo, huku milipuko ikisikika tangu alfajiri ya leo, Jumapili, karibu na Mji wa Michezo, kusini mwa mji mkuu, Khartoum.

Hali ya isiyoeleweka inaendelea kutanda kuhusu yanayojiri katika medani ya vita kutokana na taarifa zinazogongana zinazotolewa na pande hasimu. Baadhi ya taarifa zinaeleza kuwa, hadi sasa watu zaidi ya 56 wameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 600 kujeruhiwa katika mapigano hayo ya ndani.

Habari za kugongana zinahusiana zaidi na Kamandi Kuu ya jeshi la Sudan ambapo mshauri wa kisiasa wa Vikosi vya Radiamali ya Haraka ameiambia televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar kwamba: Mapigano makali yanaendelea ndani ya makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi, na kwamba maafisa wengi wamejiunga na kikosi hicho. Hata hivyo, msemaji wa Jeshi la Sudan amekanusha kile alichokiita madai ya waasi ya kuzingirwa kwa Kamandi Kuu mjini Khartoum.

Mvutano kuhusu utawala wa kiraia

Mapigano hayo yalizuka baada ya mvutano kuhusu pendekezo la kuanzishwa utawala wa kiraia na kuunganishwa vikosi vyote ndani ya jeshi moja la taifa.

Jeshi la Sudan na wapinzani wake, Rapid Support Forces (RSF), wanadai kudhibiti uwanja wa ndege na maeneo mengine muhimu mjini Khartoum na miji mingine ya nchi hiyo, ambako mapigano yameendelea usiku kucha.

Mapigano ya sasa nchini Sudan ni kati ya vitengo vya jeshi vinavyomtii kiongozi mkuu, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na vikosi vya RSF, vinavyoongozwa na naibu kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti.

Kila upande miongoni mwa pande hizo unautuhumu upande wa pili kwa kushambulia makao yake. Kile kinachojiri hivi sasa nchini Sudan ni vita vya kuwania madarakani kati ya pande mbili.]

Mkwamo wa kisiasa

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, yanayojiri hivi sasa nchini Sudan ni matokeo ya mkwamo wa kisiasa katika nchi hiyo. Mapigano hayo yamezuka siku mbili baada ya indhari ya jeshi la Sudan ambalo lilitangaza kuwa, baada ya vikosi vya radiamali ya haraka kuwekwa katika mji mkuu na miji mingine muhimu nchi hiyo sasa ipo katika "hali ya hatari". Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, hitilafu kati ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni Mkuu wa Baraza la Utawala Sudan na naibu kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo, Naibu Kiongozi wa Baraza la Utawala Sudan zilikuwa zimeongeza uwezekano wa kuibuka makabiliano baina ya jeshi na vikosi hivyo. Katika majuma ya hivi karibuni, jeshi la Sudan na kikosi cha radiamali ya haraka vilikuwa vimekusanya wanajeshi na silaha katika mji mkuu Khartoum pamoja na viunga vyake.  Kabla ya hapo pia, jeshi la Sudan lilikuwa limeimarisha uwepo wake katikati ya Khartoum na lilikuwa limeweka magari ya kivita takribani katika maeneo yote yanayoishia katika ikulu ya Rais.

Mapinduzi ya kijeshi

Sudan imekuwa bila serikali ya kiraia tangu Oktoba 2021 wakati jeshi lilipofuta serikali ya mpito ya Waziri Mkuu, Abdalla Hamdok, na kutangaza hali ya hatari, hatua iliyopingwa na vyama vya kisiasa ambavyo viliitaja kuwa "mapinduzi ya kijeshi."

Kwa sasa Jenerali Abdul-Fatah al-Burhan kamanda wa jeshi ndiye kiongozi wa Sudan akiwa kiongozi wa Baraza la Utawala wa Mpito.

Disemba mwaka jana (2022) kulifikiwa makubaliano baina ya makundi ya kiraia na Baraza la Utawala wa Kijeshi kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa Sudan.  Pande hili ziliafikiana kuhusu kipindi cha mpito cha miezi 24. Mapatano hayo ambayo yanahesabiwa kuwa msingi wa utatuzi wa mgogoro wa kisiasa wa Sudan yalisainiwa huko Khartoum na makundi ya kiraia na baraza la Uongozi wa Mpito la Sudan kwa kuhudhuriwa na viongozi wa ndani, kikanda na kimataifa.

Kuzidi kuwa mbaya hali ya kiuchumi na kijamii ya Sudan, kuendelea kushuhudiwa mkwamo wa kisiasa na kuongezeka ukosoaji kutokana na utendaji wa Baraza la Utawala hususan hatua yake ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel sambamba na juhudi za wazi na za tangu kabla za Abdul-Fatah al-Burhan za kuimarisha utawala ni mambo ambayo yaliwafanya watu wataraji kuibuka tena vita vya kuwania madarakani katika nchi hiyo ya Kiafrika.

4134499

Kishikizo: sudan jeshi al burhan
captcha