IQNA

Vita

Mapigano Sudan yaua watu 578, UN yasema nchi inasambaratika

18:51 - April 30, 2023
Habari ID: 3476936
TEHRAN (IQNA)- Mapigano kati ya wanajeshi wa Sudan yameingia wiki yake ya tatu ambapo hadi kufikia leo watu zaidi ya 578 wameuawa huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa nchi hiyo inasambaratika.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Jumamosi kwamba mzozo wa kuwania madaraka kati ya makamanda wawili wakuu wa vikosi vya Jeshi la Sudan, na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vinasambaratisha nchi hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Hakuna haja ya kuendelea kupigania madaraka wakati nchi inasambaratika," akizungumzia mapigano yanayoendelea kati ya Mkuu wa Jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambayi pia ni mtawala wa Sudan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemeti, ambaye anaongoza RSF.

Guterres, ambaye alikuwa akizungumza na kituo cha televisheni cha Al Arabiya baada ya juhudi za kuongeza mapatano ya saa 72 kushindikana, ametilia mkazo juhudi zinazoongozwa na Waafrika za kupatanisha pande hizo mbili, akisema, "ombi langu ni kwamba kila kitu kifanyike kuunga mkono mpango wa amani nchini Sudan unaoongozwa na nchi za Afrika.”

Pia, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilitoa tahadhari, likionya kwamba ghasia zinazoendelea zinaweza kutumbukiza eneo la mashariki mwa Afrika katika janga la kibinadamu.

Kwa sasa kuna uhaba wa chakula, maji, na mafuta katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, ambako mamilioni ya watu wamenaswa.

Sudan, kwa miongo kadhaa, imekuwa ikitawaliwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja na serikali ya kijeshi na majenerali hao wawili walichukua madaraka katika mapinduzi ya 2021 ambayo yaliondoa mpito wa Sudan kuelekea utawala wa kiraia wa demokrasia na hatimaye kumfanya waziri mkuu, Abdullah Hamdok ajiuzulu.

Hamdok alionya siku ya Jumamosi kwamba mzozo uliopo unaweza kuingia katika mgogoro wa kimataifa, mkubwa kiasi kwamba matatizo yanayosababishwa na vita vya Syria, Yemen, au Libya yantaonekana kuwa madogo ikilinganishwa na yatakayojiri Sudan.

Hamdok, ambaye alijiuzulu Januari mwaka jana, alisema mzozo katika taifa hilo la Afrika unaweza kuzorota na kuwa moja ya vita mbaya zaidi vya wenyewe kwa wenyewe duniani ikiwa hautasimamishwa mapema.

Tangu kuzuka kwa mzozo wa Sudan, zaidi ya watu 578 wameuawa na zaidi ya 4,000 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.

3483382

Kishikizo: sudan vita dagalo burhan
captcha