IQNA

Matukio ya Sudan

Mapatano ya kusitisha mapigano Sudan yakiukwa sikuu ya Idul Fitr

22:19 - April 22, 2023
Habari ID: 3476903
TEHRAN (IQNA)- Mashambulizi ya mara kwa mara yalirindima katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum hata baada ya pande mbili hasimu kutangaza kusitisha mapigano

Umoja wa Mataifa, na mataifa mengine kadhaa yamesema yanafanya maandalizi ya kuwaondoa raia wao nchini humo baada ya takriban wiki moja ya ghasia.

Mamia wameuawa na maelfu wamejeruhiwa tangu mapigano makali yalipozuka Jumamosi kati ya vikosi vinavyomtii mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan ambaye pia ni mtawala wa nchi hiyo na naibu wake, Mohamed Hamdan Dagalo, kamanda wa kikosi chenye nguvu cha msaada wa dharura (RSF) ambaye ni maarufu kwa jina la Hemeti.

Vikosi vinavyoongozwa na majenerali hao wawili waliokuwa washirika katika baraza tawala la Sudan vilianza mapigano mkali wa kuwania madaraka wikendi iliyopita. Hali ni mbaya nchini humo na Umoja wa Mataifa unasema taifa hilo linalotegemea msaada wa chakula sasa linakaribia kutumbukia katika janga la kibinadamu.

Milio ya risasi iliendelea mjini Khartoum siku ya Ijumaa, ingawa mapigano hayakuwa makali kama siku za awali. Mapigano hayo ya jana ni pigo kwa jitihada za  kimataifa za kutaka uhasama usitishwe.

Mahasimu wote wawili, Jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), walitoa taarifa  walikubaliana kuhusu suluhu ya siku tatu ili kuwawezesha wananchi kusherehekea sikukuu ya Idul Fitr iliyoanza jana nchini humo.

Taarifa ya Jeshi la Sudan ilisema, "Vikosi vya jeshi vinatumai kuwa waasi watatii matakwa yote ya usitishaji vita na kusimamisha harakati zozote za kijeshi." Hivi karibuni Jeshi la Sudan limetangaza kuwa kikosi cha RSF ni kundi la waasi.

Askari wa jeshi la kitaifa na wapiganaji wa RSF walifyatuliana risasi siku nzima jana ikiwa ni pamoja na wakati wa Sala ya Idul Fitr wakati wa asubuhi.

Shirika la Afya Duniani siku ya Ijumaa liliripoti kuwa watu 413 wameuawa na 3,551 kujeruhiwa tangu mapigano yalipozuka siku sita zilizopita nchini Sudan. Idadi ya waliofariki ni pamoja na wafanyakazi watano wa kutoa misaada.

RSF ni kikosi chenye nguvu kilichoundwa na wanamgambo wa Janjaweed ambao kwa miaka mingi walihusika katika mapigano ya mkoa wa magharibi wa Darfur.

Shirika la Kimataifa linaloshughulikia mizozo, ICG, limesema hatua za haraka zinahitajika ili kusitisha ghasia zinazoweza kugeuka kuwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, na kuonya kwamba hali ya kutisha ambayo wengi waliihofia nchini Sudan ndiyo inayoshuhudiwa kwa sasa. 

4135792

captcha