IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu /37

Nabii Zakariya; Msaidizi Mkuu wa Kwanza wa Nabii Isa

15:18 - April 25, 2023
Habari ID: 3476911
TEHRAN (IQNA) – Makuhani wengi walitoa tuhuma zisizo sahihi dhidi ya Bibi Maryam baada ya kuzaliwa kwa Isa Masih (Yesu) na wakati huo Zakariya aliibuka na kuwa msaidizi na muungaji mkono wa kwanza wa Bibi Mariamu na Nabii Isa-Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-(AS).

Zakariya ni mmoja wa Mitume wa Bani Isra’il. Alikuwa mkuu wa makuhani na watumishi katika al-Quds (Jerusalem), akiwalingania watu kwenye dini ya Nabii Musa.

Kuna maoni tofauti kuhusu ukoo wake; wengine wanaamini kuwa alikuwa mtoto wa Barkhiya, mmoja wa wajukuu wa Hazrat Yaqub. Wakati huo huo, wengine wanaamini kwamba Zakariya anaweza kufuatiliwa hadi kwa Musa. Mtazamo mwingine ni kwamba yeye ni dhuria wa Hadhrat Sulaiman.

Barkhiya alikuwa miongoni mwa viongozi wa dini wakati huo, akiishi Palestina. Wanahistoria wanasema Zakariya pia alikuwa seremala. Mke wake, Elizabeti, alikuwa shangazi ya Bibi Maryam.

Kulikuwa na dada wawili mashuhuri katika Bani Isra’il; Anne na Elizabeti. Dada hao waliolewa na Imran na Zakariya kwa taratibu. Baada ya kifo cha Imran, Zakariya alichukua ulezi wa Maryam.

Zakariya na Elizabeti hawakupata watoto kwa miaka mingi hadi Mungu alipowajalia mtoto wa kiume aliyeitwa Yahya.

Makuhani wa Kiyahudi walipotoa shutuma zisizo sahihi dhidi ya Bibi Maryam, Zakariya alipinga madai hayo na kumuunga mkono. Wakati huo huo, baadhi ya watu walijaribu kumuua Zakariya.

Alipojua kuhusu mipango yao ya uhasama, alikimbia na kujificha katika mti. Kundi la watu binafsi liliugundua mti huo na kuukata vipande vipande na kumuua Zakariya.

Jina lake limetolewa mara saba katika sura za Qur'ani za Maryam, Al-Imran, Al-An’am, na Al-Anbiya. Kama Waislamu, Wakristo pia wanaamini utume wa Zakariya lakini Wayahudi wanaukana kwa vile wanamchukulia Zakariya kuwa kuhani wa Kiyahudi mwadilifu.

Vyanzo vingine vinasema alikuwa na umri wa miaka 130 alipofariki. Inasemekana kuwa alizikwa huko al-Quds lakini pia kuna kaburi huko Aleppo (Halab), Syria ambalo linahusishwa na yeye.

 

captcha