IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu /32

Suleiman; Nabii na Mfalme ambaye alikuwa na mamlaka maalumu

14:45 - February 20, 2023
Habari ID: 3476590
TEHRAN (IQNA) – Baada ya kifo cha baba yake Dawoud (AS), Suleiman (AS) akawa nabii na mfalme wa Bani Isra’il.

Alimwomba Mwenyezi Mungu ampe nguvu zisizo na kifani. Mwenyezi Mungu alikubali ombi la Suleiman (AS) na akamfanya kuwa mtawala wa sio tu wanadamu bali pia upepo, majini na aliweza pia kudhibiti mashetani.

Suleiman (AS) alikuwa mtoto wa Dawoud (AS) na dhuria wa Yahuda, mwana wa Yaqub (AS). Anaelezwa kuwa ni mtu aliyekuwa na uso mweupe na mwili mkubwa. Alichukua nafasi ya Dawoud baada ya kifo chake. Kulingana na vyanzo vya kihistoria, alikuwa kati ya miaka 13 na 22 wakati huo.  

Suleiman ni miongoni mwa watu wa kihistoria waliokuja kuwa nabii na mfalme. Alimwomba Mungu ampe ufalme ambao hautapewa mtu yeyote baada yake. Mungu alikubali ombi lake na akampa Suleiman uwezo ambao haujapewa mtu yeyote kabla au tangu hapo, na kumwezesha kuwa na udhibiti wa upepo, ndege, majini na mashetani. Pia, ardhi ya Bani Isra’il zilistawi chini ya utawala wake.

Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu, Mtume Suleiman (AS) alikuwa na uwezo maalum. Kwa mfano, alipewa udhibiti wa migodi ya shaba, alijua lugha ya wanyama na alikuwa na mamlaka juu ya wanadamu na pia majini na shetani. Wakati wa utawala wake, majengo mengi, kama vile Hekalu la Suleiman, yalijengwa. Kwa mujibu wa Hadithi, majengo hayo yalijengwa na majini.

Kuna hadithi nyingi zilizosimuliwa kuhusu Nabii Suleiman (AS), ikiwa ni pamoja na uwezo uliowekwa kwenye pete yake, kuzungumza kwake na mchwa na ndege wanaojulikana kama Hud Hud ( hoopoe), zulia lake lililokuwalikipaa angani na kisa cha Suleiman na Malkia wa Saba (Sheba).

Suleiman (AS) aliamuru maandishi ya wachawi na waganga yakusanywe na kuwekwa mahali maalum. Baada ya kifo chake, baadhi ya watu walichukua maandishi na kuanza kuyatumia katika mafundisho.

Suleiman (AS) alitawala Bani Isra’il kwa miaka 40. Alikufa akiwa ameegemea fimbo yake. Hakuna aliyejua kuwa amekufa kwani alibaki amesimama, akiiegemea. Kisha mchwa wakatafuna fimbo hiyo, hadi, mwishowe na mwili wake ulipoanguka watu waligundua  kuwa alikuwa ameaga dunia.

Qur'ani Tukufu inataja jina la Suleiman (AS) mara 17, ikijumuisha katika Sura Al-Baqarah, An-Nisa, Al-An’am, Al-Anbiya, An-Naml, Saba na Saad.

Katika vitabu vitakatifu vya Kiyahudi jina la Suleiman (Suleiman) pia limetajwa sana. Sulemani anahesabiwa kuwa ndiye aliyeandika vitabu vya Mithali, Mhubiri, na Wimbo Ulio Bora katika Agano la Kale.

Kwa mujibu wa Agano la Kale, Suleiman (AS) alikua muabudu masanamu mwishoni mwa maisha yake lakini Qur'ani Tukufu inasisitiza kwamba alikuwa muumini wa Mungu Mmoja hadi dakika ya mwisho na hakuwahi kuwa mshirikina.

 

captcha