IQNA

Vita vya Sudan vyaingia mwezi wa tatu; idadi ya vifo na wakimbizi yazidi kuongezeka

8:49 - June 17, 2023
Habari ID: 3477145
Vita vya Sudan vimeingia mwezi wa tatu Alkhamisi iliyopita wakati idadi ya vifo ikipindukia 2,000 na baada ya gavana wa jimbo hilo kuuawa katika jimbo la Darfur.

Mapigano hayo yamesababisha watu milioni 2.2 kuyakimbia makaazi yao wakiwemo watu 528,000 ambao wamekimbilia nchi jirani. Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji ambapo limeonya pia kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika nchi hiyo.

Mbali na onyo hiyo, mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu ya kiieneo na kimataiifa, nayo yameendelea kutahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu nchini Sudan na kutoa mwito wa kusitishwa vita hivyo.

Machafuko hayo yanayoandamana na ukatili mkubwa, ambayo yanawalazimisha raia kujifungia majumbani mwao, wakihofia kuuawa iwapo watatoka nje kutafuta chakula na maji, yamewafanya wanaharakati na waangalizi wa eneo hilo nje ya nchi kupiga kengele ya hatari, wakisema kinachoendelea katika eneo hilo ni mauaji ya kimbari na kikabila.

Baadhi wameonya kwamba, kama hali hiyo itaachwa bila kudhibitiwa, machafuko hayo yanaweza kuwa mabaya zaidi kuliko uasi wa Darfur ulioanza miaka 20 iliyopita na kusababisha vifo vya watu 300,000 na wengine milioni 2.5 kuyahama makazi yao, wakati serikali kuu ya Sudan ilipokipa kikosi cha RSF uwezo wa kupambana na makabila yaliyoasi yasiyo ya Kiarabu.

Vita kati ya Kamanda wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah al Burhan na hasimu wake Kamanda Mohamed Hamdan Dagalo hadi sasa vimeuwa zaidi ya watu 2,000.

Wakati huo huo watu zaidi ya milioni 2.2 wamelazimika kuhama makazi yao huko Sudan ambapo raia zaidi ya 528,000 wamekimbilia katika nchi jirani wakihofia mapigano.

Kishikizo: sudan Wakimbizi
captcha