IQNA

Ahul Bayt wa Mtume Muhammad SAW

Rais wa Iran: Bibi Fatima SA ni kigezo na shakhsia mashuhuri mpenda mageuzi

12:46 - December 27, 2022
Habari ID: 3476314
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Iran amemtaja Bibi Fatimatu-Zahra SA, binti kipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW kama kigezo cha mwanadamu na shakhsia mashuhuri aliyeleta mageuzi katika historia ya jamii ya wanaadamu.

Rais Ebrahim Raisi amesema hayo leo katika maziko ya mashahidi 200 wa Kiirani ambao utambulisho wao haujulikani, yaliyofanyika sambamba na kumbukuku ya siku ya kufa shahidi Bibi Fatima SA, ambaye pia alikuwa mke wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (AS), Imamu wa kwanza wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Raisi amesema kutambua haiba kubwa, maneno na vitendo vya mtukufu huyo kunawezekana kwa mwanadamu, lakini ni jambo zito, na kwamba mtu muaminifu ni yule ambaye maisha, kauli, na matendo yake yanaenda sambamba na kulandana.

Rais wa Iran amebainisha kuwa, ukweli, uaminifu na unyoofu wa Bibi Fatima AS ulidhihirika zaidi kwa namna alivyokufa shahidi, kwa kuwa alifikiria tu juu ya Allah Mtukufu.

Sayyid Ebrahim Raisi amesisitizia haja ya kuwa na maono na mtazamo wa mbali katika kutathmini mambo, akisisitiza kuwa upumbavu katika enzi hizi kwa kutumia vyombo vya habari hautofautiani na upumbavu enzi za nyuma,  na kwamba Bibi Fatima (SA) alisimama kidete dhidi ya ujinga na mapuuza.

Wananchi wa Iran wamejitokeza kwa wingi katika maziko ya mashahidi wao 200 waliouawa wakati wa vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu vilivyoanzishwa na utawala wa kidikteta wa Saddam wa Iraq dhidi ya dola changa wakati huo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Vita hivyo vilimalizika mwaka 1988 kwa kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita huku dikteta Saddam Hussein akishindwa kufanikisha lengo lake lolote na hakuna hata shibri moja ya ardhi ya Iran iliyokuwa imebakia mikononi mwa adui mvamizi. 

Kuhusu kuenea ufisadi, ukosefu wa uadilifu, na Ufarao-mamboleo katika dunia ya leo, Rais wa Iran ameleza kuwa: Ghasia za hivi karibuni hapa nchini zilikuwa aina fulani ya vita vya kimakundi vilivyojumuisha waungaji mkono wa magaidi wa MKO, utawala wa kifalme na ubeberu wa dunia. Raisi ameongeza kuwa, Qurani Tukufu imetuonya na kutukata tuwe makini na wale wanaoeneza uvumi kwa lengo la kuupotosha umma wa Kiislamu.

4110085

captcha