IQNA

Njama dhidi ya Iran

Wananchi wa Iran waandamana kulaani shambulio la kigaidi na ghasia

19:51 - October 28, 2022
Habari ID: 3475997
TEHRAN (IQNA)- Wananchi wa jiji la Tehran na miji yote ya Iran, leo baada ya Sala za Ijumaa, wamefanya maandamano makubwa ya nchi nzima kulaani shambulio la kigaidi lililotokea juzi Jumatano katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh ya mjini Shiraz, kusini magharibi mwa Iran. Genge la kigaidi la ISIS limetangaza kuhusika na jinai hiyo.

Maandamano hayo ya leo mchana ya baada ya Sala za Ijumaa, yamefanyika kwa wakati mmoja na kushirikisha watu wa kada zote wa kona zote za Iran.

Ni vyema kukumbusha hapa kwamba, watu wasiopungua 15 wameuawa huku 27 wakijeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi la juzi Jumatano yapata saa 12 kasorobo jioni kwa majira ya hapa Iran katika Haram Tukufu ya Shah Cheragh mjini Shiraz, katika mkoa wa Fars wa kusini magharibi mwa Iran.

Hadi hivi sasa nchi mbalimbali duniani zimeshatoa mkono wao wa pole kufuatia shambulio hilo la kigaidi. Miongoni mwa nchi hizo ni Russia, China, Uturuki, Pakistan, Armenia, Jamhuri ya Azerbaijan, Misri, Imarati, Venezuela, Oman, Syria, Iraq, Finland, Umoja wa Mataifa, harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Kataib Hizbullah ya Iraq, Ansarullah ya Yemen n.k, zimetoa mkono wa rambirambi kwa serikali na taifa la Iran kufuatia jinai hiyo iliyofanywa na genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh, (ISIS).

Shambulio hilo la kigaidi limetekelezwa katika hali ambayo katika wiki za hivi karibuni maadau wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametumia nguvu zao zote za kisiasa na vyombo vya habari kwa lengo la kuchochea ghasia na machafuko hapa nchini. 

Uzoefu wa miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu unathibitisha wazi kuwa maadui daima wanatumia mbinu tofauti zikiwemo za ugaidi, kuchochea machafuko na ghasia na kutumia mashinikizo makubwa ya kisiasa na kiuchumi kwa shabaha ya kuzuia kufikiwa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja na kufikiwa maendeleo na kuimarisha umoja na mshikamano nchini.

Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanadhani kwamba kupitia vitendo hivyo vya ugaidi wanaweza kuizuia Iran kufikia malengo yake ya Mapinduzi ya Kiislamu huku wakiwa wameghafilika na ukweli kwamba taifa la Iran daima limekuwa likidumisha malengo na njia ya mashahidi na bila shaka damu ya mashahidi imawasaidia pakubwa katika kuendeleza njia hiyo tukufu inayoidhaminia Iran malengo yake matukufu.

Ni wazi kwamba jinai iliyotekelezwa hivi karibuni na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku nchi zinazodai kutetea haki na kupambana na ugaidi zikiwa zimenyamaza kimya, kwa mara nyigine tena imeanika wazi unyama na uovu wa nchi hizo na vibaraka wao. Kama alivyosema Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, maadui wameamua kutumia ugaidi dhidi ya taifa la Iran ili kulipiza kisasi cha pigo kubwa walilopata na kushindwa kufikia malengo yao maovu nchini, lakini pamoja na hayo watambue kwamba vyombo vya usalama na polisi nchini watawafuatilia kwa makini wahusika wa jinai ya hivi karibuni na kuwaadhibu vikali wapangaji na watekelezaji wote wa jinai hiyo.

4094999

captcha