IQNA

Fikra za Kiislamu

Nini Maana ya Imani?

21:47 - October 08, 2022
Habari ID: 3475899
TEHRAN (IQNA) – Wakati mwingine watu hawaamini wanachokiona bali wanajaribu kupata elimu na imani inayohitajika ili kupata uhakika wa kile walichokiona.

Kwa kifupi, uhakika huo ndio huitwa  "Iman" au imani katika Uislamu. Inakua ndani ya moyo na ni zaidi ya kile kinachoonekana.

Kuna maoni kadhaa juu ya maana halisi ya "Iman" kwani inaweza kumaanisha amani, uthibitisho, ukosefu wa woga, na kuwa na uhakika wa jambo fulani.

Kwa kuzingatia kipengele cha kidini, Iman maana yake ni kuwa na imani ya kina kwa Mwenyezi Mungu, Mtume SAW, na chochote alichokileta. Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, mifano ya Iman ni kuamini Mwenyezi Mungu, Mitume, yaliyoteremshwa kwa Mitume, Siku ya Kiyama, Malaika, na ghaibu.

Baadhi ya watu wameuchukulia Uislamu na Imani kuwa ni kitu kimoja lakini wengine wanaamini kuwa viwili hivyo ni tofauti. Qur'ani Tukufu inabainisha kwamba imani ina thamani na nafasi ya juu zaidi ikilinganishwa na Uislamu: "Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. (Surah Al-Hujurat, aya ya 14)

Uislamu na Imani zina viwango kadhaa kwani ngazi ya kwanza ya Uislamu ni kukubali maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kiwango cha kwanza cha Iman ni kuwa na imani kubwa ya Tauhidi, utume na maamrisho ya Uislamu.

Imani inaweza kutiwa nguvu au kudhoofika: “Inapoteremshwa Sura (ya Qur’an) baadhi ya watu huwauliza wengine, “Ni imani ya nani miongoni mwenu iliyopata nguvu kutokana na (ufunuo huu)? Hakika (wahyi) inatia nguvu imani ya Waumini na wanaichukulia kuwa ni bishara njema."  (Sura At-Tawbah, aya ya 124)

Na imani huleta faraja kwenye nyoyo: “Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua! ” ( Sura Ar-Ra’d, aya ya 28)

Wakati huohuo, hakuna mtu anayeweza kulazimishwa kutafuta imani: “Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. ” (Surah Al-Baqarah, aya ya 256)

Kwa hiyo, kadiri watu wanavyoweza kufikia kiwango cha Iman, wanaweza pia kutoka katika eneo hili na hivyo kuna ulazima wa kulinda Imani ili isalie kuwa imara: “ Hakika walio amini, kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha wakazidi ukafiri, Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaghufiria wala wa kuwaongoa njia. (Sura An-Nisa, Aya ya 137)

captcha