IQNA

Mufti wa Moscow aunga mkono hatua ya Rais Putin kuhusu Ukraine

22:47 - February 23, 2022
Habari ID: 3474965
TEHRAN (IQNA)- Mufti wa Moscow alionyesha kuunga mkono uamuzi wa Rais wa Russia Vladimir Putin wa kutambua maeneo yaliyojitenga ya Lugansk na Donetsk mashariki mwa Ukraine kama jamhuri huru.

Sheikh Albir Krganov alisema hatua hiyo ni ya haki na inalinda maisha ya watu.

Amesema Waislamu wa Russia wanaelewa suala la kujitenga kwa mikoa hiyo miwili na Ukraine na wanakaribisha.

"Ninaamini uamuzi wa kutambua uhuru wa jamhuri za Lugansk na Donetsk ni wa haki," alisema, akiongeza kwamba hatua ya Russia hailengi kumdhuru mtu yeyote bali kusaidia kuzuia vifo vya raia.

Mufti Krganov alisema mazungumzo yanaposhindikana, ni lazima uamuzi ufanywe kwa sababu watu wanasubiri.

Uamuzi kama huo haukuwa rahisi lakini ulifanywa kwa kuzingatia maoni ya jamii, wataalam na baraza la usalama la Russia, alisema.

Putin Jumatatu alitia saini amri ya kutambua maeneo  hayo yaliyojitenga kama jamhuri huru, akiiambia wizara ya ulinzi ya Russia kupeleka wanajeshi katika maeneo hayo mawili.

Alitoa tangazo hilo moja kwa moja kwenye televisheni baada ya hotuba ya hisia ambapo aliitaja mashariki mwa Ukraine kama "ardhi ya kale ya Russia " na kusema "inasimamiwa na mataifa ya kigeni".

"Ninaona ni muhimu kufanya uamuzi ambao ulipaswa kufanywa muda mrefu uliopita - kutambua mara moja uhuru na uhuru wa Jamhuri ya Watu wa Donetsk na Jamhuri ya Watu wa Lugansk," rais wa Russia aliongeza.

Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekosoa vikali chokochoko za Marekani na shirika la kijeshi la NATO katika mgogoro wa Ukraine na kusisitiza kuwa, uingiliaji huo umeshadidisha taharuki mashariki mwa nchi hiyo jirani na Russia.

Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pande zote husika kwenye mgogoro huo zinapaswa kujizuia kuchukua hatua yoyote inayoweza kushadidisha hali ya mambo. Khatibzadeh alisema hayo Jumanne katika taarifa na kuongeza kuwa, "kwa bahati mbaya, uingiliaji wa mambo, na hatua za uchochezi za NATO ikiongozwa na Marekani zimefanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi katika eneo hilo."

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Tehran inafuatilia masuala yanayofungamana na mgogoro wa Ukraine kwa mazingatio makubwa.

4038291

captcha