IQNA

Oman yasisistiza kuunga mkono Palestina na kutoanzisha uhusiano na Israel

16:29 - July 10, 2021
Habari ID: 3474087
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono haki za kisheria za Palestina na katu haitafanya mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa gazeti la Ash-Sharqul- Awsat', Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Al Busaidi amesema, "sisi, katu hatutakuwa nchi ya tatu ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi itakayoanzisha uhusiano wa kawaida na Israel."

Al Busaidi amesisitiza kuhusu msimamo wa Muscat wa kuunga mkono upatikanaji wa suluhu na amani jumuishi na ya kiuadilifu kwa mujibu wa mpango wa uundaji nchi mbili na akaongeza kuwa, hilo ndilo chaguo pekee linalokazaniwa na kutiliwa mkazo na mpango wa amani wa Waarabu na jamii ya kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ameeleza pia kwamba hakuna mpango wowote uliopendekezwa na nchi yake kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Yemen na kwamba inachopigania Oman ni kufikiwa mapatano kati ya pande zote husika katika mgogoro wa nchi hiyo sambaba na kutilia mkazo kurejeshewa Syria uwanachama wake katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Al Busaidi amezungumzia pia nafasi na mchango wa Iran katika eneo na akasema, Iran siku zote imekuwa ikiunga mkono juhudi za kurejesha amani na uthabiti.

Wiki iliyopita vyombo vya habari vilizinukuu baadhi ya duru za nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na kuripoti kwamba, Sultan Haitham bin Tariq Al Said wa Oman atafanya ziara ya kuitembelea Saudi Arabia kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kadhia ya Yemen na matokeo ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran.

/3983107/

Kishikizo: oman palestina israel
captcha