IQNA

Bomu lalipuka katika msikiti Libya, watu kadhaa wajeruhiwa

14:38 - August 05, 2017
Habari ID: 3471105
TEHRAN (IQNA)-Bomu limelipuka katika mlango wa msikiti mjini Benghazi, Libya Ijumaa baada ya sala ya Alfajiri na kuwajeruhiwa watu saba.
Duru zinasema bomu lililipuka wakati waumini walipokuwa wakiondoka katika Msikiti wa Ataiwish baada ya Sala ya Alfajiri na kwamba waliotekeleza hujuma hiyo walikuwa wakimlenga Salah Al-Ataiwish, kiongozi mwenye ushawishi wa kabila la Maghariba. Al-Ataiwish ni muitifaki wa karibu wa Jenerali Khalifa Haftar kamanda wa majeshi ya Libya aliye na makao mashariki mwa nchi hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa Al Ataiwish kulengwa katika njama ya kutaka kumuua na watu wasiojulikana. Katika hujuma ya Novemba mwaka jana alijeruhiwa wakati akitoka katika msikiti huo huo bada ya Sala ya Ijumaa miezi miwili baada ya majeshi ya Haftar kuchukua udhibiti wa vituo muhimu vya kuzalisha mafuta huko Ras Lanuf and Sidra kwa msaada wa wapiganaji wa kabila la Maghariba. Haftar anafungamana na serikali na bunge la Libya lililo mashariki mwa nchi hiyo na anapinga serikali ya Libya iliyo katika mji mkuu, Tripoli ambayo unaungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Walioshuhudia hujuma ya Ijumaa wanasema bomu lilikuwa limeachwa katika eneo la kuweka viatu katika mlango wa msikiti na kwamba miongoni mwa waliojeruhiwa ni watoto wawili wa al-Ataiwish.

Tokea Oktoba mwaka 2011 baada ya kuuawa dikteta wa miaka 40 wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, Libya ilitumbukia katika machafuko na mgogoro wa kisiasa.

3626733

captcha