IQNA

Watu 14 wauawa katika hujuma ya kigaidi msikitini Iraq

17:53 - June 28, 2016
Habari ID: 3470420
Watu 14 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti mmoja viungani mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Duru za usalama na hospitali nchini humo zimesema mshambuliaji wa kujitolea muhanga mapema leo amejiripua ndani ya msikiti mmoja katika kitongoji cha Abu Ghraib, magharibi mwa Baghdad na kusababisha vifo vya watu 14. Habari zaidi zinasema kuwa, watu wengine 32 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la kigaidi. Hata hivyo, hadi tunaenda mitamboni hakuna kundi lolote lililokuwa limekiri kuhusika na hujuma hiyo. Shambulizi hilo la bomu ni la kwanza dhidi ya Iraq tangu jeshi la nchi hiyo litangaze habari ya kukombolewa kikamilifu mji wa Fallujah. Siku ya Jumapili jeshi la Iraq lilitangaza habari ya kukombolewa kikamilifu mji wa Fallujah kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Daesh ambapo wanamgambo wa kitakfiri wa kundi hilo wapatao 1,800 waliuawa kwenye operesheni ya kuukomboa mji huo wa magharibi mwa Iraq.

Itakumbukwa kuwa, wanachama wa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri waliwaua kwa kufyatulia risasi raia zaidi ya 30 magharibi mwa mji wa Fallujah katika mkoa wa al-Anbar mnamo Juni 11.

3460226

Kishikizo: iraq bomu msikiti iqna
captcha