IQNA

Utawala wa Kizayuni wazidi kupora ardhi za Wapalestina

16:23 - March 16, 2016
Habari ID: 3470200
Utawala wa Kizayuni wa Israel umenyakua kipande kikubwa cha ardhi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Unyakuzi huo mpya unakiuka sheria za kimataifa zinazoitaka iache kujitanua katika ardhi za Wapalestina.

Radio ya Utawala ghasibu Israel imetangaza Jumanne kuwa utawala huo umenyakua ekari 579 karibu na Bahari ya Chumvi au Bahari ya Mauti mjini Ariha (Jericho). Wanaharakati wa amani wanasema unyakuaji huo ni mkubwa zaidi huko Ukingo wa Magharibi katika miaka ya hivi karibini. Harakati ya Amani Sasa ambayo inapinga ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni imetoa taarifa na kusema utawala haramu wa Israel unapanga kunyakua ardhi zaidi za Wapalestina ili kujenga vitongoji na maeneo ya kitalii.

Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo inatawala eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi imetoa taarifa Jumanne na kuitaka jamii ya kimataifa iushinikize utawala wa Israel usitishe unyakuaji huo. Licha ya kupita karibu miaka 50 ya tangu Israel ilipoanza kulikalia kwa mabavu eneo la Ukingo wa Magharibi na mji wa Baytul Muqaddas, lakini hadi leo hii Israel inaendelea kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huku mirengo ya kulia na kushoto ya Israel ikishindania tenda za kufanikisha jinai hiyo. Viongozi wenyewe wa utawala wa Kizayuni wamekiri mara kadhaa kuwa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ndio mshipa wa uhai kwa Israel. Awali vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilijengwa kwenye maeneo ya mbali yasiyokaliwa na watu, lakini pole pole vitongoji hivyo vilianza kuunganishwa na vingine na kuingia hadi kwenye miji ya Wapalestina. Lengo la kujenga vitongoji hivyo ni kuvuruga muundo wa kijamii na kijiografia wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ili kuufunga mikono Umoja wa Mataifa usiweze kuainisha mipaka ya ardhi za Wapalestina na kuwalazimisha wanajeshi wa Israel kutoka kwenye ardhi hizo. Hadi leo hii, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaendelea kiasi kwamba maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Maaifa nambari 242 na 338 yanayoitaka Israel kutoka kwenye ardhi za Wapalestina bila ya masharti yoyote yanAonekana hayana maana yoyote.

captcha