IQNA

Iran yalaani vikali hujuma ya Saudia hospitalini nchini Yemen

22:21 - October 28, 2015
Habari ID: 3407236
Iran imelaani vikali hujuma ya hivi karibuni ya ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya hospitali moja nchini Yemen.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bi. Marzieh Afkham Jumatano alisema Saudia inalenga kuiteketeza kabisa Yemen katika hujuma dhidi ya nchi hiyo.  Amesema Yemen inakumbwa na hali mbaya sana ya kibinadamu kutokana na hujuma zisizo na kikomo na za kila siku za ndege za Saudia dhidi ya nchi hiyo masikini. Afkham pia ameilaumu jamii ya kimataifa kwa kutochukua hatua za kukabiliana na ukatili wa Saudia dhidi ya Yemen. Ikumbukwe kuwa siku ya Jumatatu ndege za kivita za Saudi Arabia zilidondosha mabomu mara kadhaa katika hospitali ya Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, katika wilaya ya Hidan, mkoani Sa'ada kaskazini mashariki mwa Yemen.

Mkurugenzi wa MSF nchini Yemen Hassan Boucenine amesema hospitali hiyo imeharibiwa sana kutokana na hujuma kadhaa za ndege za kivita za Saudia. Ameongeza kuwa ni wazi kwamba hujuma hiyo ya Saudia ni jinai ya kivita na kwamba hakuna sababu yoyote ya kuishambulia hospitali hiyo. Karibu watu sita walijeruhiwa katika hujuma hiyo ya Saudia.

Saudi Arabia na waitifaki wake tarehe 26 mwezi Machi mwaka huu walianzisha mashambulizi dhidi ya waanchi wa Yemen wasio na hatia  kwa kisingizio cha kuirejesha serikali ya Yemen iliyojiuzulu. Mashambulizi hayo mbali na kuharibu miundo mbinu, hospitali, misikiti, shule na nyumba za raia, yameuwa na kujeruhi pia maelfu ya watu. Karibu Wayemen 7,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa katika hujuma hizo za kinyama za Saudia nchini Yemen.

3399584

captcha