IQNA

Aya 150 za Qur’ani Tukufu kuhusu astronomia, kosmolojia

13:07 - August 10, 2015
Habari ID: 3340977
Mwanafalaki (mwanaastronomia) mashuhuri wa Iran amesema kuwa kuna aya 750 katika Qur’ani Tukufu kuhusu sayansi asilia na sayansi jarabati kwa lengo la kuwakumbusha watu masuala kuhusu maudhui kama vile maumbile ya mbingu na ardhi, milima, mimea n.k.

Katika mahojiano maalumu na IQNA, Hussein Omidian, mwanachama mwandamizi wa Jumuiya ya Falaki (Astronomia) ya Iran ameongeza kuwa kuna aya 150 katika Qur’ani Tukufu kuhusu masuala ya astronomia au falaki na kosmolojia.
Amesema wafasirina wa Qur’ani daima wamekuwa wakizingatia aya hizo na kutoa maelezo na ufafanuzi kwa mujibu wa ufahamu waliokuwa nao katika zama walimoishi.
Msomi huyo amesema katika baadhi ya aya, Allah SWT anawakumbusha watu kuhusu adhama ya maumbile ya mbingu na ardhi. Kwa mfano katika aya ya 57 ya Surat Ghaafir Allah SWT anasema: “Bila ya shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu. Lakini watu wengi hawajui.”
Katika Surat Al-Mulk, Allah SWT anawataka watu kutafakari kuhusu maumbile ya mbingu na wadiriki namna hakuna nuksani katika mfumo wa maumbile, “Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha.”
Ameongeza kuwa kadiri mwanadamu anavyostawi katika sayansi ndivyo mengi yaliyo katika Qur’ani yatakapozidi kubainika wazi.
Mtaalamu huyo wa astronomia Iran amesema ustawi wa sayansi unazidi kubaini kuwa nidhamu iliyoko katika duniani si ya mkono wa mwanadamu.
Hussein Omidian amesisitiza kuwa Qur’ani Tukufu si kitabu cha sayansi bali ni kitabu cha maisha chenye aya nyingi kuhusu maumbile kwa lengo la kuwakumbusha wanadamu kuhusu nidhamu ya uliwmengu na Muumbaji wake.
Omidian anaashiria aya ambayo mwanadamu anatakiwa kutafakari kuhusu maumbile na kuitaka aya ya 6 ya Surat Qaaf isemayo: “Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyo zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa”.
Katika aya ya 27 ya Surat Annazia’at isemayo: “Je! Ni vigumu zaidi kukuumbeni nyinyi au mbingu? Yeye ndiye aliye ijenga!”
Omidian  anaashiria aya za Qu’rani zinazoapa kuhusu nyota na hapa anangazia Surat Al-Waaqia’ah aya ya 75-74:  “Basi naapa kwa maanguko ya nyota, Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua!
Mtaalamu huyo anasema sayansi ya astronomia na kosmolojia ni ya juu sana na mwanaadamu bado yupo katika hatua za awali za kuifahamu sayansi huyo.”
Anamalizia kwa kuashiria aya za 190 na 191 za Surat Al’Imran zisemazo:
“Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili, Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto.”.../mh

3337949

captcha