Sayyid Hassan Nasrallah aliyasema hayo jana Ijumaa, katika maadhimisho ya Arubaini ya kamanda mwandamizi wa harakati hiyo ya muqawama, Shahidi Mustafa Badreddine aliyeuawa nchini Syria Mei 13 na kusisitiza kuwa, mwanamapambano huyo alikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na matakfiri wa Daesh au ISIS. Amesema Saudia na Uturuki zimetuma maelfu ya wanachama wa ISIS nchini Syria kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar al-Assad lakini njama hizo zimeambulia patupu. Kadhalika Sayyid Hassan Nasrallah amekanusha madai ya kipropaganda yanayotolewa na vyombo vya habari vya Kiarabu kwamba Hizbullah inaelekea kusambaratishwa katika eneo la Aleppo nchini Syria na kuongeza kuwa, zaidi ya magaidi 600 wameuawa kaskazini magharibi mwa mji huo mwezi huu wa Juni pekee, katika operesheni ya pamoja ya harakati hiyo ya Muqawama na jeshi la Syria.
Itakumbukwa kuwa, Mustafa Badreddine, kamanda huyo wa Hizbullah
aliyekuwa na umri wa miaka 55 aliongoza tawi la harakati hiyo ya
Kiislamu lililokuwa linaisaidia serikali ya Syria katika vita dhidi ya
magaidi. Aidha aliongoza oparesheni dhidi ya wanajeshi vamizi wa Israeli
huko Lebanon na hivyo amekuwa akilengwa kuuawa kwa muda mrefu na
Marekani, Israeli na waitifaki wao. Shahidi Badreddine alikuwa binamu
yake Imad Mughniyeh ambaye naye aliuawa shahidi katika oparesheni
iliyotekelezwa na utawala haramu wa Israel mjini Damascus, Syria mwaka
2008.
Kuhusianana yanayojiri nchini Bahrain, Sayyed Nasrallah amesema ukandamizwaji nchini humo unatakelezwa kwa amri ya Saudi Arabia.