IQNA

Misri

Mwanamuziki Misri afungwa jela miezi 6 kwa kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu

17:37 - January 29, 2024
Habari ID: 3478272
IQNA - Ahmed Hijazi, mwanamuziki wa Misri, amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa kuitusi Qur'ani Tukufu, vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeripoti.

Miezi michache iliyopita, kipande cha video kilisambazwa katika mitandao ya kijamii kikionyesha Hijazi akifundisha usomaji wa Surah Yasin ya Qur'ani Tukufu pamoja sambamba na sauti  ya Oud- ala ya muziki.

Mwanasheria aliwasilisha malalamiko dhidi ya Hijazi, akimshutumu kwa kukidharau Kitabu Kitukufu na Uislamu.

Mahakama nchini humo sasa imemhukumu mtunzi huyo wa miziki kifungo cha miezi sita jela.

Hukumu hiyo ilitolewa siku ya Jumapili, huku mahakama ikiruhusu Hijazi kulipa pauni 2,000 za Misri ili kukaa nje ya jela kusubiri matokeo ya mwisho ya kesi hiyo.

Klipu hiyo ya video, iliyosambazwa Agosti 2023, iliibua hasira na ukosoaji mkubwa miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, huku Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar na Jumuiya ya Wasomaji wa Qur'ani Misri wakilaani hatua ya Hijazi.

Kufuatia machafuko hayo, Hijazi alitoa tamko, na kuwaomba radhi watu wa Misri, Al-Azhar, jumuiya ya wasomaji Qur'ani na Waislamu wote.

Alisema hakuwa na nia ya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu ambayo alisema ni "Neno la Mwenyezi Mungu na sheria yetu kutoka kwa Mwenyezi Mmungu."

captcha