Siku ya Alhamisi, Wapalestina katika mji unaokaliwa wa Ukingo wa Magharibi wa Al-Khalil waliadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) kwa furaha katika mitaa iliyokuwa imepambwa huku kukiwa na mihadhara kadhaa ya kidini. Hata hivyo, walikabiliwa na vikwazo vizito kutoka kwa wanajeshi wa Israel karibu na Msikiti wa Ibrahim, ambao ulikuwa kitovu cha sherehe hizo za Maulidi.
Idara ya Wakfu ya Kiislamu iliandaa hafla hiyo iliyojumuisha mihadara na qasida za Kiislamu katika msikiti huo unaoaminika kuwa eneo awalimozikwa Manabii Ibrahim, Ishaq na Yaqub. Msikiti huo unaheshimiwa na Waislamu na Wayahudi na uligawanywa kati ya makundi hayo mawili baada ya walowezi wa Kiyahudi wenye itikadi kali kuwaua Waislamu 29 wa Kipalestina ndani yake mwaka 1994.
Mji mkongwe wa Al-Khalil (Hebron) pia ulipambwa kwa puto, kamba nyepesi na mabango ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW).
Ghassan Al-Rajbi, mkurugenzi wa Msikiti wa Ibrahim, amesemamsikiti huo umefunguliwa kikamilifu wiki hii kwa ajili ya waumini kusherehekea hafla hiyo. Ameongeza kuwa wanajeshi wa Israel walizidisha hatua zao za kuwakandamiza karibu na msikiti huo ili kuzuia sherehe hizo za Maulidi.
Msikiti wa Ibrahimi na mji wa kale wa Al-Khalil viliongezwa kwenye Orodha ya Turathi ya Dunia ya UNESCO mnamo Julai 2017. Al-Khalil ni mji wenye Waislamu wa Kipalestina wapatao 160,000 na walowezi 500 wa Israel ambao wanaishi katika maeneo yenye ulinzi mkali.
3485353