IQNA

Harakati za Qur'ani

Shirika la Wakfu la Libya lazindua Mus’haf Mpya

22:07 - March 20, 2023
Habari ID: 3476734
TEHRAN (IQNA) – Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) nchini Libya imezindua Mus’haf (nakala ya Qur’ani Tukufu) iliyochapishwa na Shirika la Wakfu la nchi hiyo.

Hafla ya uzinduzi ilifanyika katika mji mkuu wa Tripoli Jumamosi jioni na kuhudhuriwa na maafisa wa kisiasa na kijamii na mabalozi wa baadhi ya nchi za Kiislamu nchini Libya pamoja na wahifadhi wa Qur'ani Tukufu, miongoni mwa wengine.

Abdul Hamid al-Dbeibeh, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika hotuba yake aliangazia uungaji mkono wake kwa wahifadhi na wanaharakati wa Qur'ani Tukufu nchini humo.

Vile vile amepongeza juhudi zinazofanywa na kamati ya wataalamu wa Qur'ani Tukufu kutayarisha Mus’haf wa Kitaifa wa Shirika la Wakfu.

Muhammad al-Abani, mkuu wa shirika hilo, pia aliipongeza kamati na kusisitiza msaada wa kifedha na kiroho wa GNU kwa kukamilisha mradi huo.

Wajumbe wa kamati hiyo pamoja na Kamati ya Kitaifa ya Qur'ani walitunukiwa baadaye katika hafla hiyo.

Hapo awali ilitangazwa kuwa kamati ya Jumuiya ya Awqaf inayoundwa na Masheikh, wanazuoni na wataalamu wa Qur'ani kutoka sehemu mbalimbali za nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika, ilitumia miaka mitano kuipitia na kuichambua nakala hiyo kabla ya kutoa kibali cha kuchapishwa.

Libya ni nchi yenye Waislamu wengi Kaskazini mwa Afrika ambayo ina zaidi ya watu milioni moja ambao wameweza kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu.

Nchi hiyo imekuwa katika machafuko tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoungwa mkono na muungano wa kijeshi wa NATO mwaka 2011 kumpindua na kumuua kiongozi mkongwe Muammar Gaddafi. Imegawanywa kati ya GNU huko Tripoli na utawala wenye makao yake mashariki.

4129105

Kishikizo: libya waislamu Wakfu
captcha