IQNA

Vita dhidi ya ugaidi

Libya yawahukumu kifo magaidi 17 waliokuwa wamejiunga na Daesh

22:21 - December 20, 2022
Habari ID: 3476279
TEHRAN (IQNA)- Mahakama moja nchini Libya imewahukumu kifo magaidi 17 waliokuwa wamejiunga na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh).

Aidha mahakama hiyo ya mjini Tripoli jana Jumatatu iliwahukumu wanachama wengine 14 wa ISIS kifungo cha maisha jela, huku wengine kadhaa wakisukumwa jela kwa miaka kadhaa.

Sehemu ya hukumu iliyosomwa dhidi ya watu hao waliohukumiwa jana inasema: Mumepatikana na hatia ya kufanya vitendo vinavyohusishwa na IS, kwa kuhujumu dola na amani ya kijamii, na pia kufanya jinai kwa silaha katika mji wa magharibi wa Sabratha na viunga vyake.

Korti hiyo ya Libya ambayo haijataja uraia wa wanachama hao wa ISIS imesema, waliopatikana na hatia waliuawa watu 53, mbali na kuharibu majengo ya umma na 'kuwapoteza' makumi ya watu.

Libya imekuwa uwanja wa machafuko tangu Jeshi la Nchi za Magharibi NATO kwa kuongozwa na Marekani, kuingilia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kumuondoa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.

Tangu wakati huo, nchi hiyo imekosa usalama huku makundi ya kigaidi hususan Daesh (ISIS) yakitumia machafuko hayo kujipenyeza ndani ya taifa hilo.

3481754

captcha