IQNA

Uchaguzi wa rais Libya waakhirishwa

20:45 - December 22, 2021
Habari ID: 3474706
Maafisa wanaosimamia uchaguzi wa kwanza wa rais katika nchi iliyovurugwa kwa vita ya Libya wamethibitisha kuwa haiwezekani kuandaa uchaguzi huo Ijumaa hii kama ilivyopangwa na kupendekeza uahirishwe kwa mwezi mmoja.

Uchaguzi huo ulikusudia kuleta mwanzo mpya katika taifa hilo la Afrika Kaskazini, mwaka mmoja baada ya muafaka wa kihistoria wa kusitisha vita na zaidi ya muongo mmoja baada ya vuguvugu la mapinduzi yaliyomuondoa madarakani na kumuuwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.

Hii leo mwenyekiti wa kamati ya bunge inayofuatilia uchaguzi huo imemwambia spika wa bunge kuwa baada ya kutathmini ripoti za kiufundi, mahakama na usalama, haitowezekana kuandaa uchaguzi huo Desemba 24. Haikupendekeza tarehe mbadala ya kupigwa kura hiyo, lakini tume ya uchaguzi ya Libya imependekeza usogezwe hadi Januari 24.

Mapema mwezi huu, Omar Abdel Aziz Bushah Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Uongozi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya alitoa pendekezo la kuakhirishwa uchaguzi huo. Bushah alitoa wito  kuakhirishwa uchaguzi wa rais wa Libya hadi Februari mwaka ujao wa 2022 badala ya Disemba 24 mwaka huu.  

Hitilafu za ndani huko Libya zimezuia watu wengi kugombea katika uchaguzi ujao wa nchi hiyo. Hatua ya Saiful Islam Gaddafi, mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi na Jenerali Khalifa Haftar kujiandikisha kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi ujao imezidisha mivutano ya kisiasa nchini Libya. Saiful Islam Gaddafi anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu Vilevile Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Kijeshi ya Libya iliagiza kutiwa nguvuni Saiful Islam kwa kuhusika na mauaji na kuwatumia mamluki katika vita. Hata hivyo Mahakama ya Rufaa katika mji wa Sabha hivi karibuni iliitisha kikao maalumu kuchunguza malalamiko ya Saiful Islam Gaddafi kuhusu kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi wa rais na ikatoa dikrii na kutangaza kuwa, Saiful Islam anaweza kushiriki katika uchaguzi bila kizuizi chochote. Suala hilo limechochea mivutano na misuguano huko Libya. Akthari ya wananchi wa Libya wanaamini kuwa, mwana huyo wa kiume wa Gaddafi hafai kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais. 

3477047

Kishikizo: libya uchaguzi
captcha