IQNA

ISIS (Daesh) watishia tena kuibomoa al-Ka'aba Tukufu

12:06 - August 27, 2015
Habari ID: 3353091
Kundi la magaidi na wakufurishaji wa ISIS (Daesh) kwa mara nyingine wametishia kuibomoa al-Ka'aba katika mji mtakatifu wa Makka.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA,  tovuti ya habari ya albawabhnews.com,  imedokeza kuwa kundi la ISIS limetuma ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kudai kuwa eti Waislamu wanaabudu jiwe badala ya Allah SWT na hivyo al-Ka'aba inapaswa kubomolewa.
Kundi hilo lenye itikadi za Kiwahabi limesema likiweza kuuteka mji wa Makkah basi litaiteketeza al-Ka'aba na kuisawazisha na ardhi kwa amri ya kinara wa kundi hilo Abu Bakr al-Baghdadi.
Hii si mara ya kwanza kwa kundi hilo la wakufurishaji kutangaza nia ya kubomoa al-Ka'aba.
Mwaka jana, Abu Turab Al-Maqdisi, mwanachama mwandamizi wa ISIS katika akaunti yake ya Twitter alidai kuwa, "kwa uwezo wake Allah na uongozi wa Sheikh al-Baghdadi, tutaiteka Makka na kuwaua mahujaji 'wanaobabudu jiwe' tutabomoa al-Ka'aba.
Aliidai kuwa, "watu wanaoenda al-Ka'aba kugusa jiwe na si kuabudu Mwenyezi Mungu."
Magaidi wa ISIS wamebomoa misikiti na maeneo kadhaa matakatifu ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni katika maeneo kadhaa ya Syria na Iraq. Aidha wamebomoa makanisa na maeneo ya kale katika maeneo wanayoyashikilia.
Kundi la kitakfiri la ISIS limeteka maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Iraq na pia maeneo makubwa ya kaskazini mwa Syria. Aidha kundi hilo limechukua udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Libya huku makundi ya kigaidi ya Wilayat Sinai ya Misri na Boko Haram ya Nigeria yakitangaza utiifu kwa kinara wa ISIS. Kundi leney itikadi potofu limetekeleza jinai za kinyama katika maeneo yote linaloyakalia kwa mabavu.
Serikali ya Syria inailaumu Marekani na waitifake wake katika eneo yaani utawala wa Kizayuni wa Israel, Saudi Arabia, Qatar na Uturuki kuwa ndio waanzilishi na waungaji mkono asili wa magaidi wa ISIS.../mh

3351440

captcha