IQNA

Waislamu China

Msikiti Mkuu wa Taipei; mkubwa na mkongwe zaidi Taiwan

16:38 - January 28, 2024
Habari ID: 3478264
IQNA - Msikiti Mkuu wa Taipei, mji mkuu wa eneo la Taiwan, ni msikiti mkongwe zaidi katika kisiwa hicho na pia mkubwa zaidi.

Msikiti Mkuu wa Taipei upo katikati ya kitovu cha biashara na elimu cha jiji. Kuta zake za kijivu ni dhihirisho la enzi ya kisasa katika usanifu majengo ambao umechanganya vizuri miundo ya jadi ya Kiarabu na Kichina.

Wakiingia ndani, waumini hutembea kwenye korido ili hatimaye kufikia chumba kikubwa cha swala maombi kilichopambwa kwa mazulia na vinara. Katika pande zote mbili, mwanga wa rangi huingia kupitia madirisha ya vioo.

Msikiti huu uko katika wilaya ya Da'an na ujenzi wake ulikamilishwa mnamo 1960, na ramani yake ilichorwa  Yang Cho-cheng, mbunifu mashuhuri wa China.

Ni moja ya misikiti 11 nchini Taiwan, jimbo la watu milioni 23 kati yao elfu chache tu ya wenyeji wake ndio Waislamu.

Yaser Cheng, mwenyekiti wa Wakfu wa Msikiti Mkuu wa Taipei, anakadiria kwamba ingawa kuna Waislamu wenyeji elfu chache tu huko Taiwan, kwa ujumla kuna Waislamu wapatao 300,000, ambao ni kutoka nchi mbali mbali.

Kwa Cheng, mtu muhimu katika kuanzishwa kwa msikiti huo alikuwa Jenerali Bai Chongxi, kiongozi mashuhuri wa Kiislamu wa Uchina ambaye alikimbilia Taiwan wakati serikali ya kitaifa ya China iliposhindwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 1949.

Akiwakilisha jumuiya ya Waislamu waliohama kutoka China Bara, alipendekeza kujengwa kwa sehemu ya Kiislamu ya kuswalia yenye viwango vya kimataifa kama "lazima," Cheng alisema, akiongeza kuwa wakati wa ujenzi wa msikiti huo, Taiwan ilikuwa na uhusiano mzuri na nchi nyingi.

Katika miaka ya 1950 na 1960, mataifa mengi yalikuwa na uhusiano rasmi na Taiwan na viongozi na wanadiplomasia kutoka Mashariki ya Kati walitembelea Taipei mara kwa mara.

Wakati uwakilishi rasmi kutoka nchi tofauti umepungua tangu wakati huo kutokana na aghalabu ya nchi za dunia kufuata sera ya China Moja, mvuto kimataifa ya Taiwan haijapungua, ambayo inaonekana zaidi kwenye msikiti wake mkuu siku ya Ijumaa. Waislamu wengi wa kigeni hujihisi nyumbani katika msikiti huu katika eneo hilo lenye Waislamu wachache.

Lugha kuu zinazotumiwa katika mahubiri ni Mandarin na Kiingereza.

Taiwan ni kisiwa cha Asia ya Mashariki katika Pasifiki na ni sehemu kubwa ya eneo la Jamhuri ya China iliyoenea kwenye visiwa vingine vidogo nje ya China bara. Ingawa eneo hilo limejitangazia uhuru, China inasisitiza kuwa ni sehemu isiyotenganika na ardhi yake.

3486985

Kishikizo: waislamu china taiwan
captcha