IQNA

Rais Rouhani wa Iran

Si muhimu kwa Iran ni nani atakayeshinda uchaguzi Marekani, la muhimu ni atii sheria

19:01 - November 04, 2020
Habari ID: 3473328
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili halijalishwi wala kushughulishwa na ni nani atakayeibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani uliofanyika jana Jumanne.

Rais Rouhani amesema hayo katika kikao cha Baraza la Mawaziri hapa jijini Tehran na kusisitiza kuwa: Kile ambacho Iran inataka ni kuona serikali ijayo ya Washington inarejea katika mikataba ya kimataifa na inaheshimu sheria.

Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imechukua maamuzi muhimu katika kipindi cha wiki chache zilizopita, pasi na kujali kile kinachoendelea Marekani wala kujalishwa na ni nani ataibuka mshindi katika kinyang'anyiro cha urais nchini humo.

Rais wa Iran amebainisha kuwa: Kwetu sisi, mtu au chama si muhimu, lakini jambo la maana ni kutizama sera zitakazotekelezwa na serikali (ijayo ya Marekani).

Amesisitiza kuwa, iwapo Marekani itaweka pembeni vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na ikhitari kuliheshimu taifa la Iran, bila shaka mambo yote yatakuwa tofauti.

Mbali na Rais Rouhani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei na maafisa wengine wa Iran wamesisitiza kuwa, taifa hili halijali ni nani atakayeibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani ambao ulifanyika jana.

3933201

captcha