IQNA

Shakhsia katika Qur’ani /18

Mtihani wa Mwenyezi Mungu kwa Yakub uliodumu kwa miaka 50

16:47 - November 30, 2022
Habari ID: 3476173
TEHRAN (IQNA) – Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa watu wake wateule waliopita mitihani migumu aliyowapa. Miongoni mwa mitihani hiyo ni ile ya Yakub-Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake -(AS)- ambaye alilazimika kustahamili kutengana na mwanawe, Yusuf (AS), kwa muda wa miaka 50.

Yakub (AS) alikuwa mtoto wa Is’haq (AS) na mjukuu wa Ibrahim (AS). Alikuwa ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Habari njema za Mwenyezi Mungu za kuzaliwa kwa Is’haq na Yakub kwa Ibrahim (AS) zimetajwa ndani ya Qur'ani Tukufu.

Ishaq alikwenda katika mji uitwao Paddan Aram kwa ami yake kufanya kazi ya kuchunga mifugo huko kwa muda fulani.

Lakabu yake ni Israil na kwa mujibu wa riwaya katika vitabu vya Kiislamu na Kiyahudi, alipewa na Mwenyezi Mungu kama baraka. Israil inasemekana kumaanisha mtumishi wa Mwenyezi Mungu.

Jina la Yakub (AS) limetajwa mara 16 katika Sura 10 za Qur'ani Tukufu, na lakabu yake Israil imetajwa mara mbili katika Sura Al-Isra na Maryam.

Sheikh Tabarsi katika kitabu chake Majma’ al-Bayan fi-Tafsir al-Quran anasema Israil ni Yakub (AS) na kwamba Isra ina maana ya mja na ‘il maana yake ni Mwenyezi Mungu, na kwa hiyo maana ya Israil ni Mja wa Mungu.

Yakubu (AS) ni baba wa Bani Isra’il na wengi wa Mitume wa Mwenyezi Mungu walitokana na kizazi chake. Qur'ani Tukufu pia inatoa jina la Imam kwa Yakub (AS).

Ishaq alimsihi mwanawe Yakub kuoa msichana kutoka kwa wale wanaoishi Mesopotamia ambao walikuwa miongoni mwa walionusurika na gharika ya Nuhu. Alifanya hivyo, akaoa dada wawili walioitwa Eliya na Rahil. Alioa dada wa pili baada ya kifo cha wa kwanza.

Alikuwa na wana sita na mke wake wa kwanza Eliya, wengine wawili, yaani Yusuf na Benyamini, pamoja na Rahil, na wanne na wake zake wengine wawili.

Qur'ani Tukufu inamtaja Yakub katika hali tofauti lakini kisa cha kutengwa kwake na mwanawe Yusuf kimetolewa kwa undani zaidi katika Sura Yusuf.

Qur'ani Tukufu pia inaeleza kwamba Yakub alipofuka baada ya kulia kwa miaka mingi kwa kumkosa mwanawe, Yusuf. Kulingana na masimulizi ya kihistoria, utengano huu ulidumu kwa miaka 50.

Baada ya kumpata mwanawe tena Yakub alienda Misri na kuishi huko kwa miaka 17. Kabla ya kifo chake, Yakub aliwakusanya watoto wake wote na kuwashauri kufuata njia ya babu yake Ibrahim (AS).

Kama wajumbe wengine wa Mungu, Yakub (AS) alijulikana kwa sifa maalum. Alikuwa mtu mcha Mungu, alikuwa na ujuzi mkubwa, na alijua tafsiri ya ndoto. Ujasiri na subira yake mbele ya masaibu pia ilikuwa ya kielelezo.

Yakub alikuwa mtu wa kwanza kuingia msikitini na wa mwisho kutoka humo. Alikufa akiwa na umri wa miaka 140 au 147 na akazikwa huko Al-Khalil (Hebron), Palestina.

captcha