IQNA

Qur'ani inasema nini / 2

Mwanadamu ni Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi

14:15 - May 22, 2022
Habari ID: 3475280
TEHRAN (IQNA)- Wakati Mwenyezi Mungu SWT alipomuumba mwanadamu, alimfanya kuwa Khalifa au msaidizi wake katika ardhi.

Katika Sura Al-Baqara ya Qur'ani Tukufu aya ya 30 tunasoma hivi: "Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua."

Aya hii ni mfululizo wa aya 10 za Surah hii ambazo zinazungumza kuhusu nafasi ya mwanadamu katika dunia, sifa zake na uwezo wake. Aya hizo zinaashiria ukweli kuhusu mwanadamu kuwa Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi na kushuka kwake.

Aya hiyo inamalizika kwa kauli ya Mwenyezi Mungu kwa Malaika wake aliposema:

"… Hakika Mimi nayajua msiyo yajua."

Ni kitu gani ambacho Mwenyezi Mungu alikijua lakini Malaika walikuwa hawakijui? Wafasiri wengi wa Quran wanaamini kile malaika walichofikiri kuhusu mwanadamu ni kwa sababu kulikuwa na viumbe vingine duniani kabla ya kuumbwa kwa wanadamu ambao walifanya ufisadi.

Katika Tafsiri ya Qur'ani ya Majma al-Bayan, imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas na Ibn Masoud kwamba Malaika walijua Adam AS hatafanya dhambi na wakamuuliza Mungu swali kama hilo kwa sababu aliwaambia kwamba baadhi ya watoto wa Adam AS wangefanya ufisadi duniani.

Allamah Tabatabaei anaamini kwamba swali la Malaika lilitokana na ukosefu wao wa elimu kuhusu asili ya kidunia ya mwanadamu ambayo ni mchanganyiko wa ghadhabu na tamaa.

Lakini kuna jambo jingine zaidi ambalo Malaika hawakujua kuhusu wanadamu. Hawakujua kwamba ukamilifu wa mwisho wa mwanadamu ni kuwa Khalifa wa Mungu na njia ya kuelekea kwenye cheo hicho ni katika dunia hii. Kama alivyosema Mtukufu Mtume SAW: "Dunia ni shamba la Akhera."

Mawalii wa kipekee wa Mwenyezi Mungu pia walikuwa na viwango vya juu zaidi kabla ya kuingia katika ulimwengu huu, na katika ulimwengu huu, kulingana na kiwango hicho cha juu, walistahimili magumu na ustahimilivu katika njia ya Mungu, na kwa hiari wakadumisha nafasi zao takatifu katika ulimwengu huu.

Habari zinazohusiana
captcha