IQNA

IRIB yalaani uamuzi wa Marekani kuteka tovuti za kimataifa za habari za Iran

23:40 - June 23, 2021
Habari ID: 3474036
TEHRAN (IQNA)- Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) limetoa taarifa na kulaani hatua ya tovuti zake kadhaa na za mrengo wa muqawama kufungwa na serikali ya Marekani na kusema kitendo hicho ni ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa maoni na ni hujuma dhidi ya vyombo huru vya habari.

Taarifa hiyo iliyotolewa Jumatano imesema hatua ya Wizara ya Sheria ya Marekani imefunga  tovuti za Press TV, Al Alam, Al Kauthar , Al Masira na nyinginezo kwa visingizio visivyo vya kimantki na visivyo na msingi.

Taarifa hiyo imesema hatua hiyo inaashiria sera za kiistikbari na za kibeberu za Marekani na ni ukiukwaji wa wazi na wa makusudi wa sheria za kimataifa.

IRIB imesisitiza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter, Instagram na Youtube, imefunga akaunti za mashirika ya habari na utangazaji ya mrengo wa muqawama kwa visingizo visivyo na msingi jambo ambalo ni kinyume cha sheria za kimataifa katika uga wa uhuru wa maoni.

Taarifa hiyo imesema IRIB itatumia uwezo wake wa kisheria wa kukabiliana na kitendo hicho kiovu cha Marekani. Aidha IRIB imesema tovuti hizo zitakuwa zinatumia domain inayoishia na .ir  badala ya zile zilzofungwa ambazo zilikuwa zinaishia na .com

IRIB imesitiza kuwa itafuatilia kisheria hatua hiyo ya Marekani kukiuka uhuru wa maoni. Kufuatia hatua hiyo Press TV imetangaza kuwa tovuti iliyofungwa ya presstv.com sasa inapatikana kupitia presstv.ir

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Wakati huo huo,

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekosoa hatua ya Marekani ya kufunga tovuti kadhaa za Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) na kusema hiyo ni njama ya kuvuruga uhuru wa moani.

Katika taarifa, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema hatua ya Marekani kufunga tovuti kadhaa zilizo chini ya IRIB ni katika njama ya Washington ya kuzima sauti huru katika vyombo vya habari duniani.

Khatibzadeh, amesema hatua hiyo ni muendelezo wa undumakuwili wa sera za Marekani na kuongeza kuwa, serikali ya sasa ya Marekani inafuata ule ule mkondo wa Marekani na sera hizo hazitakuwa na natija nyingine ghairi ya kugonga mwamba.

Hali kadhalika amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itafuatilia kisheria hatua hiyo ya Marekani ya kufunga tovuti za Iran.

820043

Kishikizo: marekani iran irib presstv
captcha