IHRC imemuandikia barua Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ikimtaka amuachilie huru Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake, Bi. Mallima Zeenah.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.
Hatua kandamizi na za kikatili za polisi na jeshi la Nigeria dhidi ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky zingali zinaendelea na hadi sasa idadi kubwa ya wafuasi wa kiongozi huyo wa kidini wamewekwa kizuizini au wameuawa shahidi.
Barua aliyoandikiwa Buhari na IHRC pia inamkumbusha kuhusu mauaji ya Zaria ambayo sasa yanachunguzwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.