IQNA

Kiongozi wa Hong Kong aomba msamaha baada ya msikiti kuhujumiwa

13:13 - October 21, 2019
Habari ID: 3472182
TEHRAN IQNA)- Kiongozi wa Hong Kong amewaomba radhi Waislamu baada ya polisi wa kuzima ghasia kuuhujumu msikiti mkubwa zaidi mjini humo wakati wa kukabiliana na waandamanaji Jumapili.

Katika tukio hilo, polisi wa kuzima ghasia waliumiminia mlango wa Msikiti wa Kowloon maji ya rangi ya buluu ambayo hutumika kuwatawanya waandamanaji.

Carrie Lam Cheng Yuet-ngor ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Hong Kong , akiwa ameandamana na mkuu wa polisi Stephen Loi Wai-chung wameutembelea msikiti uliolengwa mapema leo Jumatatu katika mtaa wa Tsim Sha Tsui na kukutaana na viongozi wa jamii ya Kiislamu kuwaomba Waislamu msamaha kufuatia tukio hilo.  Katibu wa Jamii ya Kiislamu Hong Kong Said Uddin amesema mtendaji mkuu na kamishna wa polisi wamesema msikiti ulihujumiwa kimakosa na wakaahidi kuwa kosa hilo halitarudiwa tena.

Machafuko na maandamano mjini Hong Kong yaliibuka yapata miezi mitatu iliyopita katika kulalamikia mpango wa kuwarejesha watuhumiwa wa uhalifu katika eneo hilo China. Nchi kama vile Marekani na Uingereza sambamba na kushikilia bango kadhia hiyo, zimekuwa zikichochea moto wa malalamiko hayo mjini Hong Kong. Inafaa kuashiria kuwa, mji huo ulikuwa chini ya udhibiti wa Uingereza tangu mwaka 1842 hadi mwaka 1997.

Serikali ya China imeendelea kulaani vikali uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya mji wa Hong Kong, kwa kupasisha muswada uliopewa jina la 'Haki za binaadamu na demokrasia.'

3851287

captcha