IQNA

Taarifa ya Iran baada ya meli yake kushambuliwa karibu na Jeddah

20:59 - October 11, 2019
Habari ID: 3472167
TEHRAN (IQNA) - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa taarifa baada ya kushambuliwa meli ya mafuta ya Iran karibu na bandari ya Jeddah, Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu.

Katika taarifa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi amesema kuwa, dhima yote ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira uliosababishwa na kushambuliwa meli hiyo iko juu ya wanaofanya chokochoko kwenye eneo hili.

Ameongeza kuwa, uchunguzi uliofanywa na Shirika la Taifa la Mafuta la Iran unaonesha kuwa meli moja ya mafuta ya Iran leo Ijumaa asubuhi imeshambuliwa mara mbili kwenye Bahari Nyekundu katika mashambulizi yaliyopishana kwa takriban nusu saa.

Amesema mafuta yaliyokuwa yanamwagika kwenye meli hiyo yamezuiwa na Alhamdulillah hakuna mfanyakazi yeyote wa meli hiyo aliyepata madhara.

Amesema, miezi kadhaa iliyopita pia, kulitokea vitendo vya uharibifu dhidi ya meli za mafuta za Iran katika Bahari Nyekundu na uchunguzi unaendelea kufanywa ili kugundua ni akina nani waliohusika na chokochoko hizo.

Mashirika mbalimbali ya habari nayo yameripoti kuwa , mafuta yaliyokuwa yanavuja kwenye meli hiyo ya mafuta ya Iran iitwayo SABITI yameweza kudhibitiwa.

Taarifa zinasema hakuna moto wowote uliotokea kwenye meli hiyo na meli iko katika hali ya usalama na utulivu kikamilifu. Duru zinadokeza kuwa kuwa meli hiyo imeshambuliwa kigaidi yapata maili 60 kutoka bandari ya Jeddah ya Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu.

3849010

captcha