IQNA

Waislamu Buckinghamshire Uingereza wasambaza nakala za Qur'ani katika maktaba

11:06 - October 10, 2019
Habari ID: 3472165
TEHRAN (IQNA) – Imamu wa Msikiti wa Chesham huko Buckinghamshire nchini Uingereza, Sheikh Arif Hassan amezitunuku maktaba za eneo hilo nakala 20 za Qur'ani Tukufu zilizotarjumiwa kwa lugha ya Kiingereza.

Nakala hizo za Qur'ani Tukufu zilikabidhiwa Naibu Mkuu wa Kaunti ya Buckinghamshire Mark Shaw. Sheikh Arif Hussein Imamu wa Msikiti wa Chesham amesema: "Ni fahari kubwa kwa Waislamu wa Chesham kutunuku nakala 20 za Qur'ani Tukufu zilizotarjumiwa kwa Kiingereza."

Ameelezea matumaini yake kuwa zawadi hiyo itapelekea kuwepo maelewano na kuheshimiana baina ya Waislamu na wafuasi wa dini zingine.

Sheikh Arif Hussein ameongeza kuwa: "Eneo la Buckinghamshire Chiltern ni eneo la amani na wakaazi wake wanaheshimiana na hivyo ni fahari yetu kuwa hapa ni makazi yetu."

Akizungumza katika hafla hiyo Mark Shaw amesema: "Msikiti ni sehemu muhimu ya jamii ya Chesham. Kitendo hiki kilichojaa ukarimu cha Imamu na Waislamu, kitapelekea idadi kubwa ya watu waweze kuifahamu Qur'ani.

Naye Gareth William, Waziri wa Masuala ya Ushirikishi wa Jamii na Afya ya Umma ametoa  shukrani zake za dhati kufuatia zawadi hiyo kutoka kwa Msikiti wa Chesham na kusema maktaba zitanufaika pakubwa.

3469619

 

captcha