IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Silaha za nyuklia ni haramu katika Uislamu

21:41 - October 09, 2019
Habari ID: 3472163
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza msimamo imara na wa kishujaa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na uharamu wa kutumia bomu la nyuklia na kusema kuwa: Iran haiwekezi kwa ajili ya kutengeneza na kutunza bomu ya nyuklia.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo mjini Tehran katika mazungumzo yake na wasomi elfu mbili vijana na wenye vipaji vya kisayansi na kielimu wa Iran na kuongeza kuwa: "Licha ya kwamba tungeweza kupiga hatua katika njia hiyo lakini kwa kutegemea sheria za Kiislamu, tulitangaza kwamba, utumiaji wa silaha za nyuklia ni haramu; kwa msingi huo hakuna sababu ya kuwekeza kwa ajili ya kutengeneza na kutunza silaha ambazo utumiaji wake ni haramu mutlaki." 

Ayatullah Khamenei amesema miongoni mwa sifa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ni kuwapa watu wote ujasiri wa kuingia katika medani ngumu ikiwa ni pamoja na medani za sayansi, suala ambalo pia limepongezwa na maadui wa Iran. Amekumbusha fahari na mafanikio ya kisayansi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: "Utumiaji wa uwezo wa kisayansi na kielimu katika sekta mbalimbali hapa nchini umepeleka juu uwezo wa kujilinda, tiba na matibabu ya kisasa na kudhibiti magonjwa, masuala ya kiufundi ya uhandisi, bioteknolojia na uzalishaji wa bidhaa za kubakia muda mrefu kwa kutumia teknolojia ya nano, na teknolojia ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani." 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kudumishwa maendeleo ya kielimu ya Iran katika harakati inayokwenda kwa kasi ya kisayansi duniani. Ameashiria shauku na hamu kubwa, ya kupongezwa na kujiamini kwa vijana na kusema kuwa: Kila msoni kijana ni sehemu ya mwili wa Iran na kuna ulazima wa kutekelezwa na kufuatiliwa kikamilifu waraka wa kistratijia wa masuala ya wasomi ili kuweza kuondoa matatizo ya tabaka hilo hapa nchini.

Vilevile amehimiza umuhimu wa kuwepo mawasiliano baina ya wasomi wa Iran, Asia na ulimwengu wa Kiislamu na kusema: Kujenga mahusiano na wasomi wa eneo la magharibi mwa Asia, ulimwengu wa Kiislamu, kambi ya mapambano na hata kuwakutanisha pamoja wasomi wanaopigania haki duniani katika nchi zote ikiwemo Marekani na nchi za Ulaya kunaweza kuwa msingi wa kueneza elimu safi na sharifu na fikra sahihi.

/3469623

captcha