IQNA

Magaidi waua maafisa 10 wa polisi nchini Kenya

18:38 - June 15, 2019
Habari ID: 3472002
TEHRAN (IQNA) - Maafisa 10 wa polisi wameuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika kaunti ya Wajir, katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya.

Taarifa zinasema gari hilo aina ya Toyota Landcruiser lililokuwa limebeba maafisa 11 wa polisi liliripuka baada ya kukanyaga bomu hilo, katika barabara ya Khorof Harar-Konton.

Mmoja wa viongozi wa Baraza la Wazee katika eneo hilo, Abdullahi Maalim Riba amewaambia waandishi wa habari kuwa, afisa wa Polisi aliyenusurika katika hujuma hiyo ya kigaidi amewafahamishwa kuwa wenzake wote aliokuwa nao garini wameaga dunia.

Afisa huyo kwa sasa anatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Wajir. Baadhi ya duru zingine za habari zimedai kuwa ni maafisa sita tu wa polisi waliouawa katika hujuma hiyo. Magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab wamedai kuhusika na hujuma hiyo.

Jana Ijumaa, afisa mmoja wa Polisi ya Akiba aliuawa na mwanachama wa genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika eneo la Boji Qaras huko huko katika kaunti ya Wajir.

Wafuasi wa kundi la kigaidi al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia wamekuwa wakijipenyeza nchini Kenya hususan kupitia mipaka ya eneo la Kaskazini Mashariki na kutekeleza mashambulizi ya kutisha dhidi ya raia na maafisa usalama. Magaidi hao wakufurishaji wamedhoofika kufuatia oparesheni za usalama nchini Kenya lakini hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara nchini humo. 

 

3468750

captcha