IQNA

Katibu Mkuu wa UN atembelea msikiti uliohujumiwa kigaidi nchini New Zealand

17:30 - May 14, 2019
Habari ID: 3471955
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumanne hii amekutana na majeruhi na familia zilizopoteza wapendwa wao katika shambulizi la kigaidi dhidi ya misikiti miwili ya New Zealand mnamo Machi 15 mwaka huu.

Katika mkutano uliofanyika katika Msikiti wa  Al Noor Mosque, ambao ni moja ya misikiti iliyolengwa katika hujuma hizo za kigaidi, Guterres ametadharisha kuwa, matamshi ya chuki na kibaguzi yanaenea kwa kasi ya kutisha katika mitandao ya kijamii, na kusisitiza kuwa UN itaongoza jitihada za kupambana na tatizo hilo.

Amesema, "Kauli za chuki zinasambaa kama moto wa kichaka kwenye mitandao, lazima tuuzime moto huo. Hakuna nafasi ya kueneza chuki na ubaguzi kwenye mitandao au kwa njia ya moja kwa moja."

Sambamba na kuwafariji waathiriwa wa shambulizi hilo, Katibu Mkuu wa UN amewatakia kila la kheri Waislamu wa mji ulioshambuliwa wa Christchurch, wakati huu wanapotekeleza ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akiwa kwenye msikiti wa al Noor Guterres ameiambia jamii ya Kiislamu ya eneo hilo kwamba, “najua hakuna maneno ambayo yanaweza kuwaondolea maumivu, huzuni na machungu , lakini nilitaka kuja hapa binafsi ili kuwafikishia upendo, msaada na kuwashika mkono. Jamii hii inadhihirisha mshikamano ambao imeufahamu kwa muda ambao uko ndani ya Uislamu, ambao ni imani ya upendo, huruma , msamaha na huruma.”

Alikumbusha kwamba wakati akiwa kamishina mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa alishuhudia ukarimu wa nchi za Kiislam zikifungua mipaka yake kwa watu waliokuwa wakikabiliwa na madhila kutoka sehemu mbalimbali duniani ambako sehemu nyingine nyingi mipaka yao ilifungwa.

Katibu Mkuu pia amesema kwa wakati kama huu ulioghubikwa na madhila kila kona ya dunia umoja unakuwa ni nguvu kubwa akisema, “ni lazima tushikamane katika kipindi hiki kigumu. Hotuba za  chuki zinaenea na mtazamowa umma umebadilishwa. Mitandao ya kijamii inatumiwa kama jukwaa la kusambaza chuki. Lazima tuonyeshe ushirikiano katika kukabiliana na hatari hii kubwa ya chuki. "

Katibu Mkuu ameainisha mikakati miwili ambayo itasaidia kulinda maeneo ya ibada na kupambana na hotuba za chuki. Amemuomba mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya muungano wa ustaarabu Miguel Moratinos, kuandaa mpango wa hatua kwa ajili ya Umoja wa Mataifa ili kushiriki kikamilifu kusaidia kulinda maeneo ya kidini.

Pia amemuomba mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari Adama Dieng, ili kuleta pamoja timu ya Umoja wa Mataifa katika kushughulikia hotuba za chuki na kuwasilisha mkakati wa kimataifa wa hatua hizo. Amesisitiza kuwa “hotuba za chuki zinasambaa kama moto wa nyikani , ni lazima tuuzime, hakuna nafasi kwa hotuba za chuki kwenye mitandao na nje ya mitandao.”

Guterres ameishukuru jumuiya ya Waislamu wa Christchurch kwa kusaidia dunia kuwafahamu na kufahamu utu, akisisitiza kwamba katika wakati huu wa majaribu yuko hapo kuwahakikishia kwamba hawako peke yao, dunia nzima iko pamoja nao naye yuko pamoja nao.

Kila mwaka Guterres hutumbela nchi za Kiislamu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani lakini mwaka huu ameamua kutembelea New Zealand kufuatia hujuma zilizowalenga Waislamu waliokuwa wakiswali Sala ya Ijumaa mjini Christchurch mwezi Machi.

Katika shambulizi la kigaidi la Machi 200 katika misikiti ya Linwood na al-Noor mjini Christchurch, Waislamu 52 waliuawa shahidi na wengine karibu 50 kujeruhiwa. Aliyefanya unyama huo ni Brenton Tarrant, gaidi mwenye chuki na Uislamu mwenye uraia wa Australia. Gaidi Tarrant ni mfuasi sugu wa  Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni mashuhuri kwa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

 

3468519

captcha