IQNA

Wanafunzi Waislamu katika shule za Kenya walalamikia ubaguzi

12:46 - July 26, 2018
Habari ID: 3471608
TEHRAN (IQNA)- Mwenyekiti Kitaifawa Baraza la Maimamu na Wahubiri Waislamu Kenya (CIPK) Sheikh Abdalla Ateka ametoa wito kwa wizara ya elimu nchini humo kuchukua hatua za kuzuia kuendelea kubaguliwa wanafunzi Waislamu katika shule za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Sheikh Ateka ametoa wito kwa Waziri wa Elimu Bi. Amina Mohammad achukua hatua za kukabiliana na kuzuiwa wanafunzi Waislamu kutekeleza maamurisho ya Uislamu wakiwa shuleni hasa eneo la magharibu mwa Kenya.

Sheikh Ateka ametoa wito huo baada ya wazazi wa wanafunzi Waislamu kulalamika kuwa, waalimu na waalumu wakuu Wakristo katika kaunti za magharibu mwa Kenya waliwazuia wanafunzi Waislamu kuswali katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Katika barua aliyomuandikia Bi. Amina Mohammad, Sheikh Ateka amesema kwa mujibu wa katiba ya Kenya, ni wajibu kuheshimu itikadi za kimadhehebu na za kidini za watu wote, sawa wawe ni Waislamu au Wakristo. Amesema kuwazuia wanafunzi Waislamu kuswali ni sawa na kukiuka katika ya Kenya.

Mwezi Disemba mwaka jana pia, Baraza Kuu la Waislamu Kenya , Supkem, limetoa wito kwa serikali kuchukua hatua za kuzuia kusumbuliwa wasichana Waislamu wanaovaa Hijabu wakiwa shuleni.

Katika taarifa, katibu mwandalizi wa Supkem Abdullahi Salat ameitaka Wizara ya Elimu nchini Kenya kuchunguza suala la kusumbuliwa wanafunzi Waislamu wanaovaa Hijabu.

Kiongozi huyo wa Waislamu amelalamika kuwa, wanafunzi wa kike wanabughudhiwa na kudhalilishwa pamoja na kuwa mahakama imetoa hukumu ya kuruhusu wanafunzi kuvaa Hijabu wakiwa shuleni.

3732603/

captcha