IQNA

Misikiti 200 Uingereza kufungua milango kwa wasiokuwa Waislamu Jumapili

14:55 - February 14, 2018
Habari ID: 3471391
TEHRAN (IQNA)-Waliowengi nchini Uingereza wana ufahamu mdogo sana kuhusu Uislamu na kwa msingi huo, zaidi ya misikiti 200 nchini humo itafungua milango yake kwa wasiokuwa Waislamu mnamo Februari 18.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya YouGov na kufadhiliwa na Baraza la Waislamu Uingereza (MCB) unaonyesha kuwa karibu asilimia 70 ya Waingereza hawajawahi kuingia eneo la ibada la itikadi isiyo yao na kwamba asilimia 90 hawajawahi kuingia ndani ya msikiti.

Kufuatia hali hiyo, misikiti 200 kote Uingereza siku ya Jumapili, Februari 18 2018 itafungua milango kwa ajili ya kuwapokea wasiokuwa Waisalmu kwa munasaba wa 'Siku ya Kutumbelea Msikiti Wangu'. Miaka iliyotangulia misikiti kadhaa imekuwa ikiwakaribisha wasiokuwa Waislamu lakini mwaka huu utashuhudia misikiti mingi zaidi ikishiriki katika mpango huo wa kuwakaribisha majirani ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni 'Milango iliyowazi, misikiti iliyowazi na jamii zilizowazi.'

Harun Khan, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Uingereza amesema pamoja na kuwa kuna wafuasi wa dini mbali mbali nchini humo, Waingereza waliowengi hawajawahi kuingia katika eneo la ibada la wafuasi wa dini isiyo yao.

Jamii kubwa ya Waislamu Uingereza ni kutoka eneo la Asia Kusini. Aidha kuna Waislamu wengie kutoka nchi za Kiarabu, Kiafrika na pia Waislamu kutoka wa Kusini Mashariki mwa Asia, eneo la Balkan barani Ulaya na Uturuki.

Waislamu wamejitolea sana kwa ajili ya Uingereza ambapo wengi walipigana kwa niaba ya nchi hiyo katika Vita Vikuu vya Kwanza na Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Mwaka 2016 jiji la London lilimchagua Meya wa kwanza Muislamu, Sadiq Khan, aliyekuwa wakati mmoja Waziri katika chama cha upinzani cha Leba.

Kwa mujibu wa sensa ya hivi karibuni ya watu Uingereza, kuna Waislamu milioni 2.8 nchini humo kati ya watu milioni 64 nchini humo.

3465189

captcha