IQNA

Wafungwa UAE wapunguziwa vifungo kwa kuhifadhi Qur’ani

10:25 - December 10, 2017
Habari ID: 3471302
TEHRAN (IQNA)-Wafungwa 2,950 katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wamepunguziwa vifungo vyao baada ya kuhifadhi Qur’ani.

Mpango huo ambao ulizinduliwa mwaka 2001, na Sheikh Mohammed bin Rashid al Makhtoum, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa UAE ambaye pia ni mtawala wa Dubai, umechangia pakubwa kurekebisha tabia za wafungwa wengi na kuwaelimisha kuhusu urehemevu wa mafundisho ya Qur’ani.

Wafungwa pekee ambao hawawezi kupunguziwa vifungo au hukumu zao katika mpango huo ni wale waliopatikana na hatia ya kuua.

Mpango huo unasimamiwa na Taasisi ya Zawadi ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai (DIHQA) ambayo kwa muda wa miaka 16 sasa imeandaa mashindano 63 ya Qur’ani Tukufu katika magereza ya Dubai.

Kwa mujibu wa Mohammad Bu Melha, mshauri wa Mtawala wa Dubai katika masuala ya kiutamaduni ambaye pia ni mkuu wa kamati andalizi ya DIHQA anasema mpango huo wa kuhifadhi Qurani umewapa wafungwa wengi fursa ya kuanza maisha upya na kuwa raia wema kwa kutumia vizuri muda wao gerezani na baada ya kuachiliwa huru.

Takwimu zinaonyesha kuwa wafungwa wapatao 2,950 wamesamehewa au kupunguziwa vifungo vya baada ya kuzinduliwa mpango huo mwaka 2002.

Bu Melha anasema pia wanatoa zawadi za fedha na vyeti kwa wanaofanikiwa kuhifadhi Qur’ani katika viwango mbali mbali wakiwa jela. Anasema moja ya nukta ya kuvutia ni kuwa, kuna mfungwa mwanamke raia wa kigeni ambaye alisilimu na kisha kufanikiwa kuhifadhi Qur’ani kikamilifu na sasa amesamehewa na ataondoka nchini humo hivi karibuni.

3464639

captcha